Tangu kuanza kwa huduma ya uwekaji maputo tumboni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa mwaka 2023, idadi ya wawekaji wa maputo imefikia watu 128 na walioshindwa kukaa na maputo hayo ni watu watatu pekee.
Akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Agosti 10, 2023 Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi pia amesema uwekaji wa maputo tumboni anapaswa kufanywa kwa mtu mwenye uzito wa kilo 90 kwenda juu.
Amesema,“uwekaji wa maputi ni kuanzia Mtu wa kilo 90 kwenda juu, na Mtu wa juu zaidi tuliye muwekea uzito alikuwa na kilo 200 huyu ndio mtu wa juu zaidi na hao Watu watatu ambao walishindwa kukaa na puto tumboni ni kwasababu ya kutostahimili kichefuchefu, kichefu chefu kiliwazidia wakashindwa wakaja tukawatoa puto.”
Hata hivyo, Prof. Janabi amesema huduma hiyo inatolewa kwa kutumia mdomo na baada ya miezi nane huondolewa na akafafanua kwa kusema, “tunatumia mdomo kuweka puto tumboni , tunalipuliza na muda huo kuna screen inatuonyesha na tunaona linavyoingi tumboni mpaka litakapo kaa sawa.”
“Na ikitimia miezi nane unapaswa kutoa, muda huo utakuwa na mabadiliko makubwa kupitia hilo puto kwasababu linakufanya unapunguza kula, unakula kwa kiasi chako, tumemuona Msechu hivi karibuni amepungua kwa kiasi chake japo hali inakorofisha ila hali yake ya kawaida imerudi na tunaona anaendelea vizuri,” amesema Prof. Janabi.