Watu 15 wameripotiwa kupoteza maisha kufuatia vurugu za kupinga mchakato wa uchaguzi mkuu uliomalizika muda mfupi uliopita nchini Bangladesh.
Tume ya uchaguzi imeiambia Reuters kuwa imepokea malalamiko ya uchakachuaji wa matokeo katika wilaya nyingi nchini humo na kwamba itaanza kufanya uchunguzi wa malalamiko hayo wakati wowote kuanzia sasa.
Wachambuzi wa siasa za Bangladeshi wameeleza kuwa mwenendo wa uchaguzi huo unatoa nafasi kubwa kwa Waziri Mkuu, Sheikh Hasina kushinda na kuendelea na utawala wake kwa awamu ya tatu. Wakati huohuo, mshindani wake mkuu anatumikia kifungo jela kwa makosa ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Mwenendo wa uchaguzi huo ulitawaliwa na vurugu zilizofanywa na wafuasi wa vyama vya upinzani wakidai kupinga uchakachuaji. Takribani askali 600,000 walimwagwa mitaani kuhakikisha wanatuliza vurugu hizo.
Serikali iliamuru kufungwa kwa mitandao yote hadi wakati ambapo uchaguzi utamalizika ili kuepuka kusambaza taarifa za uongo na tetesi ambazo zinaweza kusababisha vurugu kubwa.
Wagombea 28 wa vyama vya upinzani walitangaza kujiondoa kwenye mchakato wa upigaji kura kwa madai kuwa wanachezewa rafu. Vyombo vya habari vimeeleza kuwa katika vituo vingi hususan katika jiji la Chittagong kulikuwa na mawakala wa chama tawala pekee.
Zaidi ya watu milioni 100 walikuwa wanatarajiwa kupiga kura leo lakini vyombo vya habari vimeripoti kuwa idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuwa ndogo.