Wakati watanzania wakisubiri kwa hamu kubwa mchezo wa mwisho wa kundi D, ili kufahamu hatma ya Taifa Stars kwenye Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ kiungo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar Baraka Gamba Majogoro, amekuwa sehemu ya wachezaji waliouzungumzia mchezo huo.

Majogoro ambae ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Taifa Stars na kushiriki fainali za CHAN, amesema wamejipanga kupambana kwa nguvu kubwa kuhakikisha wanaisasambua Guinea na kutinga hatua ya Robo Fainali.

Majogoro amesema kila mchezaji kambini kwa sasa anaufikiria mchezo huo, na anaamini kwa maandalizi waliyoyafanya chini ya kocha Ettiene Ndayiragije wataweza kuzimudu mbinu za wapinzani wao.

“Tupo tayari kwa ajili ya ushindani na tunatambua kwamba utakuwa mchezo mgumu ila hawataweza kututoa kirahisi ndani ya dakika 90.”

“Lakini siamini kama wataweza kututoa, kivyovyote vile tutapita kwenda robo fainali kwani tutapambana vya kutosha uwanjani.” Amesema Majogoro.

Stars ipo kundi D ina alama tatu baada ya kucheza michezo miwili, imeshinda mmoja kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namibia na imepoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Zambia kwenye mchezo wa ufunguzi.

Stars wamekuwa wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bonamoussadi,Douala na mchezo wa mwisho wa Kundi D kwenye mashindano ya CHAN dhidi ya Guinea unatarajiwa kuchezwa leo Jumatano, Januari 27 saa 4 usiku Uwanja wa Reunification,Cameroon.

Aweso aagiza mradi wa maji Kyaka Bunazi kukamilika kwa wakati
Bocco awahakikishia ushindi watanzania