Wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikitarajiwa kuendelea mapema mwezi ujao, Wakata Miwa wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro Mtibwa Sugar, wametangaza hali ya hatari kwa timu pinzani.
Mtibwa Sugar wametangaza hali hiyo kupitia kwa Afisa Habari wao Thobias Kifaru, ambapo amesema wamedhamiria kupambana vilivyo katika michezo ya lala salama, ili kufanikisha lengo walilojiwekea msimu huu 2020/21.
Kifaru amesema hawataki kurudia makosa yaliyojitokeza msimu uliopita, ambapo hali yao ilikua mbaya hadi kufikia hatua ya kuwa sehemu ya timu ambazo zilitarajiwa kushuka daraja.
“Tumejipanga kweli kweli, hatokuwa na huruma na timu yoyote tutakayocheza nayo katika mzunguuko huu wa pili, hatutaki yatufike kama ya msimu uliopita ambapo ilikua chupuchupu kushuka daraja.”
“Tumejizatiti kufanya vyema tukiwa na kocha wetu mpya Hitimana Thiery ambaye tayari ameshaambiwa na uongozi nini Mtibwa Sugar inahitaji katika kipindi hiki.”
Mtibwa Sugar wapo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakiwa wamecheza michezo 18, wakiwa na alama 22, zilizotokana na ushindi katika michezo 6, huku wakipoteza michezo 8 na kuambulia sare mara 4.