Uongozi wa Young Africans umetoa sababu za kuwaajiri vijana kwenye benchi la ufundi la timu yao, ambalo linaongozwa na kocha kutoka nchini Burundi Cedric Kaze.
Young Africans jana Jumatano (Januari 27) ilimtambulisha Nizar Khalifan kuwa kocha msaidizi akichukua mikoba ya Juma Mwambusi ambaye aliomba kujiweka kando kutokana na matatizo ya kiafya pamoja na Edem Mortotsi kuwa kocha wa viungo.
Khalifan alikuwa kocha mkuu wa klabu ya African Lyon inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, na pia aliwahi kucheza timu ya Mtibwa Sugar pamoja na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mshauri mkuu wa klabu hiyo kuelekea kwenye mfumo wa mabadiliko, Senzo Mbatha amesema wameamua kuwaongeza vijana kwenye benchi lao la ufundi ili kwenda na kasi ya soka la kisasa.
“Tunahitaji kuongeza thamani ya ubora katika benchi ndio maana wote ni vijana na hata kocha mkuu wetu ni kijana ili kuendana na soka la kisasa,”
“Ninaona watu ambao wamechaguliwa ni watu wazuri hivyo ni suala la kusubiri na kuona namna ambavyo tutaendelea kupambana.” Amesema Senzo.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 44 baada ya kucheza michezo 18.