Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzanian ‘Taifa Stars’ Ettiene Ndayiragije, amesema haikuwa bahati kwa timu hiyo kuweza kutinga hatua ya Robo Fainali kwenye michuano ya ‘CHAN’ inayoendelea nchini Cameroon.
Ndayiragije amesema kikosi chake kilipambana vilivyo kwenye michuano hiyo na kilioonesha nia ya kutaka kutinga hatua ya Robo Fainali, lakini sare katika mchezo wa mwisho iliwakwamisha kufikia lengo hilo.
Amesema alijipanga kuifikisha mbali Taifa Stars kwenye michuano hiyo na ndio maana katika michezo miwiwli ya kundi D dhidi ya Namibia na Guinea aliwahimiza wachezaji wake kupambana kufa na kupona.
Kocha huyo kutoka nchini Burundi pia amemlaumu mwamuzi wa mchezo dhidi ya Guinea, ambao Taifa Stars ililazimishwa matokeo ya sare na kutupwa nje ya michuano hiyo, hatua mabayo iliifanya timu hiyo kufikisha alama nne zilizoiweka kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi D.
“Haikuwa bahati yetu kusonga mbele licha ya wachezaji kupambana kusaka ushindi. Pia mwamuzi wa mchezo wetu dhidi ya Guinea alifanya makosa mengi ambayo yametufanya tutolewe.”
“Wachezaji walipambana na walifuata maelekezo yote niliowapa, kwa hakika tuna jambo tumejifunza na wakati mwingine tutawez kufanya vizuri na kusonga mbele, zaidi ya ilivyokua kwenye michuano ya CHAN ya mwaka huu.” Amesema Ndayiragije.
Benchi la ufundi la Stars lipo mikononi mwa Ndayiragije ambaye anafanya kazi kwa kushirikiana na Seleman Matola pamoja na Juma Mgunda ambao ni wasaidizi wake.
Stars ilipoteza mchezo wake wa kwanza kwa kufungwa na Zambia mabao mawili kwa sifuri, kisha ikaichapa Namibia bao moja kwa sifuri kabla ya kulazimishwa sare ya mabao mawili kwa mawili dhidi ya Guinea.
Zambia na Guinea ndizo zilizokata tiketi ya kushiriki hatua ya ribo fainali, zikitokeza kundi D.