Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk Rehema Nchimbi na viongozi wa Wilaya ya Manyoni kutatua mgogoro wa ardhi wa eneo la Majengo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ambao umesababishwa na Idara ya ardhi ya halmashauri hiyo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 31 Januari, 2021 aliposimama kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini kutoka Tabora kwenda Dodoma.
“Nimeambiwa bibi Elizabeth Sarali mwenye miaka 90 amepokonywa eneo lake kisha akamilikishwa mfanyakazi wa idara ya ardhi ambaye amepangisha Mnara wa Vodacom, hiyo hati ifutwe na arudishiwe umiliki huyo bibi aanze kulipwa pesa yake na waliopanga,”amesema.
Pia Dkt. Magufuli amemtaka mwenyekiti wa Halmashauri ya Manyoni kufuatilia kwa ukaribu taarifa kuhusu migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo ili afanikiwe kusimamia watendaji na kutatua migogoro hiyo.
”Inaonekana Mwenyekiti wa Halmashauri ya Manyoni hauna ‘information’, utadanganywa na watendaji kuhusu mambo mengi ya ardhi, shirikiana na Madiwani kutatua migogoro hii, sipendi madiwani ambao ni ‘Yes man’ kwenye kila kitu huwa sio wazuri,”amesema Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameonesha kusikitishwa na kitendo cha mwananchi mmoja wilayani humo kwenda ofisini kwa Mkurugenzi zaidi ya mara 17 bila ya changamoto yake ya ardhi kutatuliwa
”Nimesikitika huyu mwananchi ameenda kwa Mkurugenzi mara 17 bila kero yake ya ardhi kusikilizwa, hii haiwezekani, naagiza kesho aende tena na suala lake limalizike. Mara 17 ni nyingi mno hata kama angekuwa anatafuta mshkaji angekuwa ameshampata,”.
Bofya hapa…