Kocha wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Jamhuri Kiwelu Julio amelia na namna ya wachezaji wa timu ya ‘Taifa Stars’ kuwa walishindwa kujiongeza mpaka kuondolewa kwenye Fainali za Mataifa Bingwa ya Afrika ‘CHAN’ baada ya kutoka sare ya mabao mawili kwa miwili dhidi ya Guinea.
Stars iliondoshwa kwenye fainali hizo juma lililopita kwa kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi D, kufuatia sare hiyo dhidi ya Guinea, ambayo ilitanguliwa na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Namibia, huku ikipoteza dhidi ya Zambia kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri.
Julio amesema wachezaji wa Taifa Stars walipaswa kujiongeza kwenye mchezo dhidi ya Guinea na siyo kila kitu kumuachia kocha ili waweze kuibuka na ushindi.
“Tunaweza kuwaona makocha wabovu au hawafai, mwalimu anafundisha mbinu na ufundi kuna muda wachezaji wanatakiwa wabuni wenyewe kwa kujiongeza ili waweze kushinda lakini siyo kila kitu mwalimu apige kelele,” amesema Julio.
Katika mchezo huo Stars ilipata nafasi ya kuongoza kwa mabao mawili kwa moja, kabla ya Guinea kupata bao la kusawazisha ambalo liliwavusha kwenye hatua ya makundi.