Mshauri wa Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Crescentius Magori, amesema klabu hiyo iliwahi kuwa na mipango ya kutaka kumsajili mshambuliaji mpya wa Young Africans Fiston Abdulrazack.
Magori ambaye aliwahi kuwa afisa mtendaji mkuu wa Simba SC alifichua siri hiyo mwishoni mwa juma lililopita alipohojiwa kwenye kipindi cha ‘Kurasa Za Mwisho’ cha Azam TV.
Magori alisema Simba SC ilimuona mshambuliaji huyo kwenye michuano ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Challenge’ iliyoungurumanchini Kenya miaka minne iliyopita.
“Fiston tulitaka kumsajili baada ya kumuona kwenye michuano ya Chalenji liyofanyika nchini Kenya kwenye Jiji la Nairobi na Nakuru. Ile michuano ambayo Zanzibar aliingia fainali mwaka 2017.”
“Alikuja na timu ya Taifa ya Burundi. Tayari tulishakuwa kwenye nafasi nzuri, lakini akapata ofa nono zaidi kwenda nchini Angola, kwa hiyo tulimkosa kidogo tu.” Alisema Magori.
Kuhusu madai kuwa klabu ya Simba imekuwa ikichukua wachezaji ambao timu nyingine (hususan Young Africans) zimeshaonyesha nia ya kuwasajili, hivyo kuonekana hawana jicho zuri la kuangalia wachezaji mpaka timu zingine zimtaje, Magori alikanusha uvumi huo.
“Si kweli, hawa wachezaji wote unaowaona wanacheza humu humu Afrika na sisi tunawaona. Sema sisi huwa hatuongei. Tunaongea baada ya usajili,” alisema Magori.
Alisema kuwa hata wachezaji Luis Miquissone kuwa baadhi ya klabu wanadai kuwa walitaka kumsajili, lakini wao wakawahi kitu ambacho si kweli, kwani Miquissone wao ndiyo walioanza kumuona kwenye mechi ya kwanza kati ya Simba dhidi ya UD Songo iliyochezwa nchini Msumbuji na kuanza naye mazungumzo.
“Sisi tulianza kuzungumza naye kabla hata hajaja hapa kwenye mechi ya marudiano. Hata Benard Morrison jina lake nililetewa kabla hajaenda Yanga, lakini tatizo rekodi zikaonyesha kuwa hajacheza muda mrefu, tukasubiri kwanza acheze atakakokwenda kucheza kwa miezi sita ili tumuone kwanza.”
“Yeye mwenyewe aliipenda sana Simba baada ya kuiona ikicheza Simba Day dhidi ya Asante Kotoko mwaka 2017,” alisema Magori