Shughuli ya uokoaji, ya kutafuta miili na manusura wa tetemeko la ardhi lililoikumba Indonesia na kusababisha vifo vya watu 182 pamoja na kujeruhi maelfu wengine zimeingia siku ya pili huku kukiwa na matumaini ya ufanikishaji wa zoezi hilo.
Matumaini yamepatikana kufuatia mitambo ya kufukua vifusi, malori na vifaa vya uokozi kufika eneo la tukio usiku wa kuamkia leo (Novemba 22, 2022), kwenda eneo la kitongoji cha Cianjur lililopo kusini mwa mji mkuu Jakarta ambalo limeathiriwa zaidi.
Mamlaka za usalama nchini humo, zimesema zaidi ya watu 300 wamejeruhiwa vibaya, 600 wamepata majeraha madogo na bado haijafahamika idadi halisi ya watu ambao hawajulikani walipo.
Tetemeko hilo, lenye ukubwa wa kipimo cha ritcher 5.6 liliporomosha majengo, kuharibu miundombinu na kuwafukia watu chini ya vifusi vikubwa vya udongo hali iliyopelekea kutokea kwa vifo hivyo vya watu 182.