Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeongeza muda wa siku moja kwa ajili ya kutoa nafasi zaidi kwa wapiga kura wa tuzo za muziki Tanzania ambao wameonekana kushiriki kwa wingi siku hizi za mwisho kuelekea kilele cha tuzo hizo Aprili 2, 2022.

Hayo yamesemwa leo Machi 31, 2022 na Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Matiko Mniko  kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari ambapo amesema kuongezwa kwa siku hiyo kunatokana na wapenzi wengi wa muziki kuendelea kufurika kupiga kura zaidi katika siku hizi za mwisho.

Licha ya kuongezwa kwa muda wa kupiga kura, siku ya utolewaji wa tuzo hizo inabaki kama ilivyopangwa April 2, 2022 itakayofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

“Siku ya kwanza tulitangaza kuwa mwisho wa zoezi la upigaji wa kura itakuwa leo tarehe 31,3,2022 saa sita usiku lakini kutokana na watu wengi kuonyesha uhitaji katika mchakato huu tumeona tuongeze siku moja  kutokana na majukumu waliyonayo ili waweze kushiriki na kuwachagua  wasanii wao wanaowapenda,” amefafanua Mniko

Ameongeza kwa kusema kuwa tangu kuanza kwa zoezi la upigaji kura Machi 20 mwaka huu, tayari zaidi ya mashabiki wa muziki  90,000 wameshapiga kura.

Awali, mwisho wa kupiga kura ilikuwa ni Machi 31, 2022 majira ya saa sita usiku, ambapo kwa sasa imesogezwa mpaka April 1, 2022 saa sita usiku.

Habari Picha:Rais Samia akiongoza kikao ca kamati kuu pamoja na halmashauri kuu ya CCM taifa
Kinana kumrithi Mangula