Serikali imeeleza kuwa wastani wa pato la kila Mtanzania umeongezeka katika kipindi cha mwaka mmoja kati ya 2018 na 2019.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Juni 13, 2019 kuwa hadi mwishoni mwa mwaka jana wastani wa pato la kila Mtanzania lilikuwa Sh. 2.3 milioni kwa mwaka lakini hadi Juni, 2019 ni Sh. 2.4 milioni.
Kutokana na takwimu alizozitoa waziri huyo mwenye dhamana ya Fedha na Mipango, kwa wastani pato la kila Mtanzania limeongezeka kwa Sh. 100,000.
Dkt. Mpango ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya uchumi wa Taifa katika mwaka 2018 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka wa Fedha 2019/2020.
Amesema kuwa ongezeko hilo ni sawa na wastani wa asilimia 5.6 kwa kulinganisha kipindi cha mwaka 2018 na nusu ya mwaka 2019.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango ameeleza kuwa hali ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika dhidi ya Dola ya Marekani.
Amesema kuimarika huko kumetokana na utekelezaji wa sera ya fedha, usimamizi imara wa matumizi ya Serikali na matumizi ya gesi asilia badala ya kutegemea mafuta yanayoingizwa nchini.