Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema Mikutano ya Kimataifa inayofanyika hapa nchini ni fursa ya kutangaza Lugha adhimu ya Kiswahili ambayo ni mojawapo ya Lugha Rasmi ya Kikazi ya Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Jumuiya kadhaa za Kikanda Barani Afrika.
Ndumbaro ameyasema hayo Oktoba 7, 2023 jijini Arusha katika kikao cha Maandalizi ya Mkutano wa 77 wa Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 20 hadi Novemba 9, 2023 jijini Arusha.
Amesema, Tanzania ina Wataalamu katika tafsiri na ukalimani hivyo wana uwezo wa kutoa huduma ya ukalimani katika Mikutano hiyo.
Kikao hicho kimeongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Pindi Chana na kuhudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Haroun Suleimani.