Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, kwa kushirikiana na
Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa, Askari mgambo pamoja na vyombo vingine vya
dola, imefanya operesheni maalum mkoani Mara hususani katika kanda maalum ya Tarime Rorya kwenye bonde la mto Mara.

Operesheni hiyo, iliyofanyika kuanzia Oktoba 2 – 8, 2023, imefanikisha uteketezaji wa jumla ya hekari 807 za mashamba ya bangi, ukamataji wa gunia 507 za bangi kavu iliyo tayari kusafirishwa, gunia 50 za mbegu za bangi pamoja na kuteketeza
viwanda viwili vidogo vilivyokuwa vikitumika kuchakata na kufunga bangi kabla ya
kusafirishwa ambapo watuhumiwa wawili wanashikiliwa kuhusika na dawa hizo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema wakazi wa eneo hilo wamelifanya bonde la mto Mara kama eneo maalum kwa ajili ya kilimo cha bangi na kujimilikisha kwa kutoruhusu mtu yeyote asiye mkazi kuingia kwenye bonde kama sehemu ya kuficha uhalifu wao na kutishia kumdhuru yoyote atakayeingia ndani ya bonde hilo bila ridhaa yao ikiwemo kufunga ofisi ya kijiji wakimtuhumu Mtendaji wa Kijiji cha Nkerege kutounga mkono kilimo cha bangi.

Askari wakifyeka moja ya shamba la bangi katika Operesheni iliyofanyika wilayani Tarime – Mara.

“kitendo kinachofanywa na wananchi waliopo katika eneo la mto Mara ni kinyume na sheria, viongozi wa serikali na wananchi ambao sio wakazi wa hapa hawaruhusiwi kabisa kuingia eneo la bonde ili mtu avuke anatakiwa kujieleza nia na madhumuni ya kuvuka kuelekea upande wa pili, na wahusika wasiporidhika na maelezo hawakuruhusu kuendelea na safari,” amesema Lyimo.

Ameongeza kuwa, baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa vijiji vinavyopakana na
bonde hilo pamoja na wananchi waliojimilikisha bonde hilo muhimu kwa uchumi wa taifa, wamekuwa wakikodisha na kuuza mashamba ya kulima bangi ndani ya hifadhi ya bonde hilo.

Aidha, kutokana na mto Mara kuwa muhimu sana katika ikolojia ya mbuga ya Serengeti, Kamishna Jenerali Lyimo ameomba Wizara zinazohusika kushirikiana na Mamlaka kutokomeza kilimo cha bangi katika eneo hilo, kwani mbali na operesheni
iliyofanyika bado mashamba ya bangi ni mengi pembezoni mwa mto na wananchi
wamekuwa wakitumia maji ya mto kumwagilia.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo.

“Tukiacha kilimo cha bangi kiendelee hivi, na kuwaacha wananchi waendelee kuchepusha maji ya mto kumwagilia bangi mwisho wa siku itaharibu ikolojia katika mbuga ya Serengeti na mto kwa ujumla. Ni vema tukashirikiana kuhakikisha eneo hili linasimamiwa vema ili kufanikisha kusitishwa kwa kilimo cha bangi” amesisitiza Lyimo.

Pia, Kamishna Lyimo amesema, Mamlaka kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mara
na uongozi wa wilaya ya Tarime, watafanya mikutano ya hadhara na kufikiria kuwa na
mipango kabambe kuona ni namna gani bonde litalindwa dhidi ya kilimo cha bangi na
uhalifu mwingine.

Naye diwani wa kata ya Tulwa Mheshimiwa Chacha Machugu amesema, viongozi wa serikali
za mitaa wanaosaidia kuendelea kwa kilimo cha bangi wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa watu wengine huku akiwaomba viongozi wa dini kusaidia kuwaambia waumini wao kuwa dawa za kulevya hazitakiwi.

Akizungumzia operesheni iliyofanyika, Isaya Banda mkazi wa Tarime, ameiomba
serikali kufanya operesheni endelevu katika maeneo yote ili kutokomeza bangi kwani
vijana wengi wameathirika na matumizi ya dawa hizo. Pia, amewaomba wananchi
kuwafichua wanaojihusisha na kilimo na biashara ya bangi.

Tanzania, India zasaini hati 14 za makubaliano
Tanzania, India sasa ni Washirika kimkakati