Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amepiga marufuku Wanafunzi kucheza nyimbo zisizo na maadili na kuwataka Walimu kuwa wasimamizi wa tabia za Wanafunzi Shuleni.
Mkenda amesema hayo nje ya Bunge jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu picha ya video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonesha Wanafunzi wakicheza wimbo wa Mwanamuziki mmoja wa kizazi kipya.
Amesema, “tumeshatambua shule yenyewe iko Tunduma, kulikuwa na kikundi kimeenda kutoa msaada shuleni pale, baada ya kutoa msaada ule kikaweka na muziki halafu Wanafunzi wakacheza na maudhui ya muziki wenyewe kila mtu ameusikia sina haja ya kuurudia.”
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amempongeza Profesa Mkenda kwa kukemea kitendo hicho na kutoa wito kwa watoa huduma wa watoto kusimamia malezi kwani ni jukumu la kila mmoja.