Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, Wilayani Babati Mkoani Manyara imewafikisha Mahakamani watu watatu ambao ni Watumishi wa Serikali kwa tuhuma za utakatishaji fedha, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Kesi hizo zimesomwa Kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ,Martini Massao na kusimamiwa na waendesha mashtaka Johnson ndibalema na Eveline huku watuhumiwa hao wakiongozwa na Afisa Ardhi Msaidizi, Iddi Issa.
Issa anatuhumiwa kujipatia fedha kwa njia yaidanganyifu kinyume na kifungu cha 301 cha sheria ya kanuni ya sura ya 16 Kama ilivyorejewa mwaka 2022 na utakatishaji fedha shilingi milioni 84 kinyume na kifungu cha 12 na 13 cha sheria ya utakatishaji fedha sura ya 423 mapitio ya mwaka 2022.
Mshtakiwa namba mbili na namba tatu ambaye ni Joseph Selukele na Julian Rubuka wenyewe wanakabiliwa na kesi ya kugushi barua ya malipo ya viwanja zaidi ya saba kinyume cha sheria namba 333,335 na 337 sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019 kosa lingine ni matumizi mabaya ya madaraka ya kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuiya na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Kesi nyingine ni ya kuisababishia mamlaka husika hasara kinyume na aya ndogo ya 10(1) na kifungu cha57(1) na kifungu cha 60 (2) cha sheria ya uhujumu uchumi na uhalifu sura ya 200 marejeo ya mwaka 2019 inayomkabili Joseph selukele na Juliani Rubuka .
Hata hivyo, kesi hiyo imeahirishwa hadi November 21, ambapo mshtakiwa namba mbili na tatu wameachiwa kwa dhamana na mshtakiwa namba moja amekosa dhamana kutokana na kesi yake ya utakatishaji fedha ambayo haidhaminiki.