Kiungo wa klabu ya Union Touarga ya Morocco, Eric Mbangossoum mwenye umri wa miaka 23, amevunja mkataba na klabu hiyo, hatua ambayo itakuwa rahisi kwa wekundu wa Msimbazi Simba kuipata saini yake kwa urahisi, katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Licha ya Simba SC kuwa na uhitaji wa mchezaji huyo, itaingia vitani na Wydad Casablanca na RS Berkane ambao pia wameonyesha nia ya kuwania saini ya kiungo huyo mkabaji.
Awali taarifa zilieleza kuwa Kocha Mkuu wa Simba SC Abdelhak Benchikha alitajwa kumuhitaji kiungo huyo ‘mkata umeme’ ili kuongeza nguvu katika kikosi chake na kuifanya timu hiyo kuwa na muunganiko mzuri eneo la kati hadi mbele.
Kwa mujibu wa meneja wa kiungo huyo ambaye hakutaka jina lake lianikwe hadharani amethibitishia kuwa mchezaji wake amevunja mkataba na klabu hiyo ya Morocco, na kwa sasa yupo sokoni kupitia dirisha dogo la usajili.
“Ofa ni nyingi na Simba SC ni miongoni mwa timu zinazomtaka pamoja na Wydad na RS Berkane zote zimeonyesha nia ya kumhitaji kiungo huyo ambaye anaitumikia timu ya taifa ya Chad,
“Siwezi kuzungumza ni ofa gani ambayo ni kubwa kwetu kwani huuni muda wa usajili, timu yoyote ambayo itafanya ushawishi mzuri na kumhakikishia mchezaji wetu kupata nafasi ya kucheza itakuwa na faida kubwa ya kumpata.” amesema meneja huyo
Habari kutoka ndani ya klabu ya Simba SC zinasema kwa sasa mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo na Eric baada ya Benchikha kuwaeleza anamuhitaji mtu huyo kwenye kikosi chake.
Kwa muda mrefu, Simba SC imekuwa na uhitaji wa kiungo mkabaji atakayeweza kuwaongezea nguvu mabeki wa kati licha ya kuwasajili na kuwatumia viungo kadhaa wa nafasi hiyo akiwamo Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin kwa nyakati tofauti, lakini wameonekana hawampi kocha kile ambacho anakitaka.
Pia inaelezwa kitendo cha kumkosa Kanoute katika mchezo wa juzi Jumanne (Desemba 19) dhidi ya Wydad ya Morocco kufuatia adhabu ya kadi tatu za njano, , ilimvuruga Benchikha na kuwasisitiza mabosi wa klabu hiyo kufanya usajili huo haraka iwezekanavyo.
Kukosekana kwa Kanoute kuliifanya Simba SC kusaliwa na viungo wakabaji wawili pekee Mzamiru na Ngoma ambao wamekuwa wakitumika mara kwa mara.
Erick Alizaliwa Mei 26, 2000 katika jiji la N’Djamena, na alianza kucheza soka la ushindani mwaka 2017 aliposajiliwa Racing Bafoussam ya Cameroon kwa msimu mmoja kabla ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Chad akiwa na Elec-Sport mwaka 2018 na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa msimu huo.
Pia amecheza soka la kulipwa katika klabu ya Futuro Kings ya Guinea ya Ikweta na mwaka 2020 alitua rasmi Union Touarga ya Morocco akisaidia kuipandisha daraja na kwenye soka la kimataifa kwa timu yake ya taifa ya Chad, alianza kuichezea tangu mwaka 2019 alipoitwa kwa mara ya kwanza na kucheza mchezo wa kuwania Fainali za Kombe la Dunia chini ya Kocha Emmanuel Tregoat dhidi ya Sudan na timu hiyo kulala 3-1.
Kiungo huyo anasifika kwa kutumia miguu yote miwili, kukaba kwa kutumia akili mbali na umahiri wa kutoa pasi kiufundi na kuituliza timu pale inaposhambuliwa akisaidia ukuta wa timu ndani ya timu ya taifa na hata anapokuwa kwenye majukumu ya kuitumikia klabu.