Kocha kutoka nchini Ureno Jose Mourinho amekiri angependa kuona Arsenal ikishinda taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu 2023/24, lakini Manchester City na Liverpool ndizo zenye ushindani wa kweli.
Washika Bunduki hao wanaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya mechi 17, wakiwa wamekaa kileleni kwa tofauti ya alama moja mbele ya Liverpool na Aston Villa, huku mabingwa watetezi City wakipitwa kwa alama tano.
Akizungumza kwenye kipindi cha John Obi Mikel ‘The Obi One Podcast’ Kocha huyo wa AS Roma, aliulizwa mawazo yake kuhusu nani atashinda taji la England mwaka huu.
“Naweza kusema City ina asilimia 51 na Liverpool asilimia 49,” alijibu Mourinho.
Alipoulizwa mara ya kwanza kuhusu matumaini ya Arsenal, Mourinho alijibu tu: “Nah!”
“Ushindani tofauti, ningependa washinde,” aliongeza.
“Ni kweli, Chelsea haitashinda. Haina swali. Bila shaka, Manchester United haitashinda pia. Kwa hiyo ni kati ya hizi tatu, ingawa mimi ningependa Arsenal washinde.
Wakati akiwa Kocha wa Tottenham Hotspur, Mourinho alizungumza vyema kuhusu kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, akiwataka Washika Bunduki hao kusimama naye wakati wa kipindi kigumu.
“Nataka kumpa neno zuri Mikel kwa sababu alitupa mchezo mgumu sana,” amesema Mourinho kuhusu Arteta baada ya Spurs kuishinda Arsenal 2-0 Desemba, mwaka 2020.