Mlinda Lango wa Tabora United John Noble amesema mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans, utawapa nafasi ya kuonyesha ubora wao, ambao umekuwa ukizungumzwa na mashabiki wao kila kukicha.
Tabora United italuwa mwenyeji wa Young Africans katika mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumamosi (Desemba 23) kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Mlinda Lango huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Enyimba ya nchini kwao Nigeria, amesema kama wachezaji ni wazi wanatambua ugumu uliopo ila wamejipanga ipasavyo kukabiliana na wapinzani wao kwa lengo la kupata alama tatu.
“Kila mchezo ni mgumu kama iliyopita na sisi wachezaji jukumu letu ni kuhakikisha tunapambana kwa ajili ya timu, hii ni nafasi nyingine ya kuonyesha ukubwa tuliokuwa nao kwa sababu uwezo na uzoefu tunao wa kukabiliana na yoyote,” amesema.
Noble ameongeza licha ya kutoka kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao hutumiwa kwa michezo yao ya nyumbani na kuhamishiwa Jamhuri mkoani Dodoma, ila haitowaathiri kwa kiasi kikubwa kutokana na ukaribu wa miji hiyo japo wanawakosa Mashabiki wao halisia.
“Young Africans ina wachezaji wazuri na siwezi kusema mmoja wao aliyekuwa hatari kwa sababu naona wanacheza kitimu zaidi na kila mtu ana morali anapopata nafasi ya kucheza hivyo itakuwa mechi ngumu lakini tutapambana kadri ya uwezo wetu kushinda” amesema
Mchezo huu utakuwa ni wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa timu hizi kukutana tangu Tabora United ilipopanda rasmi msimu huu ambapo katika michezo 12 iliyocheza imeshinda mitatu, sare sita na kupoteza mitatu ikishika nafasi ya 10 na pointi 15.
Mara baada ya mechi hiyo, Tabora United itajiandaa kwa mchezo mwingine dhidi ya Simba SC uliopangwa kupigwa Desemba 29, japo kuna hatihati ya kuchezwa kulingana na kuwepo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, itakayoanza rasmi Desemba 28 Visiwani Zanzibar.