Kiungo kutoka nchini Denmark na klabu ya Manchester United, Christian Eriksen, huenda akawepo kwenye benchi wakati wa mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya West Ham keshokutwa Jumamosi (Desemba 23).
Eriksen alifanya mazoezi na wachezaji wenzake kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo baada ya Man United kupambana na kuambulia sare 0-0 dhidi ya Liverpool mwishoni mwa juma lililopita, huku kiungo huyo akitarajiwa kukipa nguvu kikosi cha Erik ten Hag.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31, alikuwa nje ya dimba tangu alivyoumia majuma matano yaliyopita, wakati wa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Luton.
Kutokuwepo kwa Eriksen kikosini, Man United ilipata tabu eneo la safu ya kiungo cha ushambuliaji, hivyo kurejea kwake ni taarifa njema kwa mashabiki wa timu hiyo.
Aidha, mkongwe wa klabu hiyo, Paul Scholes anaamini ujio wake utaongeza nguvu baada ya mwendo usioridhisha wa timu hiyo katika mechi zao za hivi karibuni.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha TNT, Scholes alisema: “Nafikiri Christian Eriksen na Casemiro wakirejea wataongeza nguvu kwenye timu, wachezaji hawa wana uzoefu sana, matumaini yangu wacheze wote, mambo yatakuwa sawa kwa Ten Hag.”
Hata hivyo, licha ya Eriksen kurejea kikosini, kocha Ten Hag atakuna kichwa kwa ajili ya mechi dhidi ya West Ham, kwani hana uhakika kama atakuwa fiti asilimia 100.
Wakati huo huo, Casemiro, Tyrell Malacia na Lisandro Martinez wameondolewa kwenye kikosi kitakachosafiri kwenda London kwa ajili mchezo huo, huku Harry Maguire, Mason Mount, Victor Lindelof na Amad Diallo watakosekana.