Shirika la Afya Duniani – WHO liliwahi kuonya kuwa maisha ya watu yamo hatarini kutokana na takribani watu 130,000 kukabiliwa na baa la njaa katika Pembe ya Afrika na kwamba uwezekano wa raia kufikwa na umauti au maradhi kwa jamii utafuata isipochukuliwa tahadhari.

WHO, ilitoa tahadhari hiyo huku ikisema watu wapatao milioni 48 kwenye nchi za Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini na Uganda wanakabiliwa na viwango vikubwa vya ukosefu na uhaba wa chakula.

Meneja matukio wa Shirika la WHO wa Pembe ya Afrika , Liesbeth Aelbrecht alisema watu hao wanakabiliwa na njaa huku hatari ya magonjwa na vifo vikiwanyemelea na kutaka nchi wahisani kuhakikisha wanachukua hatua za dharula kusaidia hatua hiyo.

Aelbrecht ambaye alikuwa akiongea na Waandishi Habari mjini Geneva kwa njia ya video kutoka Nairobi, naye aliongeza kuwa kati ya watu 129,000, watu 96,000 kati yao wapo nchini Somalia na 33,000 katikia Taifa la Sudan Kusini.

Alidai kuwa, maeneo mengi katika ukanda huo yanapambana na ukame mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 40, huku yakiathiriwa kwa mafuriko na kwamba ongezeko la miripuko ya magonjwa limeshuhudiwa na idadi kubwa ya watoto wenye utapiamlo.

Pamoja na tahadhari hiyo kutolewa, hali katika ukanda huo na maeneo mengine bado ni tete huku Mataifa mengi yakijielekeza kwenye majanga mapya kwa kiasi kikubwa na hali za waathiriwa inaendelea kuzorota.

Majanga ya mafuriko, vita, matetemeko ya ardhi na hata mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yamekuwa yakiendelea kutokea, yamefanya Nchi wahisani kuyageukia ili kutoa usaidizi na kuyapa kisogo mazonge ya zamani.

Bila shaka zinahitajika njia thabiti za mgawanyo wa majukumu katika kuhudumia nchi athirika kulingana na matukio husika na si kuhudumia kwa mfumo wa kigeugeu, kwani uangaliaji wa majanga mapya usifanye ya zamani yakasahaulika, kwani itasaidia kuondoa uwezekano wa vifo na uwepo wa maradhi ya waathiriwa.

Uchaguzi DRC: Raia washindwa kupiga kura Goma
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 22, 2023