Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara umerudi tena kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Kitanzania, Simon Msuva ukitaka kufanya mpango wa kumsajili haraka kupitia dirisha dogo baada ya kuachana na klabu ya JS Kabylie ya Algeria.
Msuva ametemwa Kabylie sambamba na mshambuliaji mwingine mkongwe, Hichem Mokhtar kutokana na viwango vyao kutomvutia kocha Luis Almeida, raia wa Ureno.
Tangu kocha huyo atue Kybalie, Msuva alishindwa kuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza kutokana na mfumo wa Mreno huyo kumkataa hivyo kwa muda mrefu alikuwa akitokea benchi na wakati mwingine kukosekana kabisa kikosini kwa kuishia kukaa jukwaani tu kama mtazamaji.
Lakini kutemwa kwa nyota huyo za zamani wa Moro United, Young Africans, Difaa El Jadida na Wydad Casablanca imekuwa ni kama kurahisishiwa kazi kwa mabosi wa Young Africans waliokuwa wakiisaka saini yake tangu katika dirisha kubwa lililofungwa Agosti 31 mwaka huu kabla ya mwenyewe kuibukia JS Kabylie.
Kutokana na hali hiyo Yanga kwa mara nyingine tena imejitosa mapema kuwania saini ya Msuva har- aka ikitaka kumrudisha klabuni hapo ili aje kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.
Habari za Msuva kuachana na Kabylie, imekuwa ni njema kwa Young Africans kutokana na ukweli klabu hiyo kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kusaka mshambuliaji mwenye makali kuja kuongeza nguvu kikosi hicho kilichofunga jumla ya mabao 30 katika Ligi Kuu Bara kupitia michezo 10 tu.
Mabosi wa Young Africans waaamini kuwa Msuva licha ya kutemwa na Kabylie bado ana nguvu ya kuja kufanya kitu ndani ya kikosi chao.
Imefahamika kuwa, bosi mmoja mzito wa juu wa Young Africans amewasiliana na Msuva akimtaka kufikiria haraka kujiunga na klabu hiyo ya zamani hiyo wakati akitafuta akili mpya.
Kabla ya kuondoka nchini, Msuva aliipa Young Africans mataji kadhaa na pia kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu misimu miwili tofauti.