Nyota wa zamani wa Paris Saint-Germai na SSC Napoli, Ezequiel Lavezzi amenusurika kufa baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali, kwa mujibu wa ripoti.
Taarifa zimeripoti kiungo huyo wa zamani wa Argentina ambaye alistaafu kucheza soka mwaka 2020, alipelekwa hospitali va Maldonado kwa ajili ya kupatiwa matibabu haraka.
Haikufahamika jeraha la Lavezzi mwenye umri wa miaka 38, amelipataje kwa mujibu wa vyanzo vya habari vilivyotolewa huko Uruguay tukio lilikotokea.
Hata hivyo, familia yake imesema Lavezzi aliteleza kutoka juu ya ngazi na kuanguka chini wakati anafunga taa.
Lakini polisi wameripoti kuwa nyota huyo wa zamani wa PSG alichomwa kisu na mtu mmoja kutoka kwenye familia yake wakati wa sherehe huku chanzo cha ugomvi kikitajwa kuwa ni masuala ya pesa.
“Hakuna ripoti kamili, na maendeleo ya hali ya Lavezzi bado hayafahamiki mpaka sasa,” taarifa ya polisi iliyotolewa kwa vyombo vya habari ilieleza.
Inadaiwa Lavezzi alivunjika mfupa wa shingo, huku moja ya vyanzo vingine vya habari vikidai nyota huyo wa zamani wa SSC Napoli alidondoka na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
Kwa mujibu wa FM Gente, kituo cha redio kilichopo Maldonado, Lavezzi alipelekwa hospitalini na mpenzi wake na kulazwa.
Lavezzi aliichezea Napoli kuanzia msimu wa 2007-2O12 na kuifungia mabao 38, kabla ya kujiunga na I’SG mwaka 2012 na kudumu nayo hadi mwaka 2016 akiifungia mabao 22.