Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdilhak Benchikha amesema ataendelea kutoa nafasi kwa wachezaji wanaojituma si kwa kuangalia jina wala umaarufu wao.
Pia amemtaka kila mchezaji kutimiza wajibu wake ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa katika mashindano yote wanayoshiriki.
Benchikha amesema yeye ni kocha mwenye kusimamia misingi na kuamini kile kinachofanywa na mchezaji uwanjani bila kujali kama watachelewa kupata mafanikio.
“Nitaendelea kusimamia kauli yangu ya kutoangalia jina la mchezaji, ninachotaka kwenye kikosi changu ni kila mhezaji awajibike kutimiza malengo ya timu, Simba SC ni timu kubwa na kila mchezaji ana uwezo ndiyo maana yupo hapa,” amesema Benchikha.
Amesema kwa siku dhache ambazo amekaa na timu hiyo amebaini uwezo mkubwa wa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa hawatumiki lakini chini ya utawala wake atahakikisha anawajengea ari na kujiamini ili kuwatumia katika mechi zijazo za mashindano yote.
Amesema alianza kufanya hivyo kwenye mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ambapo aliwapa nafasi wachezaji watatu ambao tangu wasajiliwe hawajacheza hata mchezo mmoja.
Benchikha amewaomba viongozi na mashabiki kumpa ushirikiano katika mpango wake ambao lengo ni kutengeneza timu bora isiyotegemea uwepo wa mchezaji mmoja au wawili.