Baada ya kumaliza kibarua kizito katika mashindano ya kimataifa, uongozi wa klabu ya Simba SC umetamba nguvu zote wanazielekeza katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Jumanne (Desemba 19) walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wake wa Mzunguuko wanne wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad AC, mechi iliyofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Baada ya kumaliza mchezo huo Simba SC inarejea katika mechi zake za Ligi Kuu ambapo kesho Jumamosi (Desemba 23) itashuka dimbani kumenyana na KMC, kisha itacheza na Mashujaa FC na kumaliza dhidi ya Tabora United kabla ya kwenda Zanzibar kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi na kurejea katika mashindano ya kimataifa Februari, mwakani kumalizia mechi zake mbili dhidi ya Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema wametoka katika majukumu ya kimataifa na sasa wanarejea katika ligi ili kupigania nafasi ya kwanza katika msimamo.
Amesema kuwa wanajua wanaenda kucheza mchezo wao wa kwanza dhidi ya KMC na timu hiyo siyo ya kuibeza kwani ina wachezaji wazuri lakini anaamini kikosi chao kitapambana kuhakikisha wanapata ushindi.
Ahmed Ally amesema anaamini wachezaji wao kwani wana morali yakutosha kuelekea katika mchezo huo kwani kikubwa wanataka kupata ushindi katika kila mechi.
“Unajua tumetoka katika mechi za kimataifa lakini wachezaji wetu bado wana morali yakutosha kuelekea katika mchezo huo, tumejipanga vyema kuhakikisha hatupotezi kwani tunazihitaji pointi tatu za KMC” amesema Ahmed Ally.
Kocha wa KMC, Abdihamid Moalin amesema kikosi chao kinaendelea na maandalizi ya kusaka alama tatu katika mchezo wao dhidi ya Simba.
Moalin amesema KMC inajipanga kukabiliana na Simba SC, anaarmini mchezo utakuvwa mgumu lakini kikasi chake hakitabweteka na kukubali kipigo.
“Maandalizi yanaendelea na ninajua mchezo utakuwa mgumu dhidi ya Simba SC ambayo imetoka kufanya vizuri, timu yangu nayo inataka kufanya vyema hivyo tutapambana hadi dakika ya mwisho,” amesema Moalin.
Kocha huyo ameongeza kuwa, ana timu nzuri ambayo inaendelea kupambana katika ligi na kutafuta matokeo mazuri.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 22 ikishinda mechi saba, sare moja na kupoteza mchezo mmoja baada ya kushuka dimbani mara tisa huku KMC wao wapo nafasi ya tano ikiwa na alama 20 ikiwa imeshinda mechi tano huku ikitoka sare michezo mitano na kupoteza mechi tatu baada ya kucheza mechi 13.