Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Kamishna Mwandamizi wa Polisi Ramadhan Ng’azi amepiga marufuku uwepo wa magari mabovu Barabarani huku akisema hatua kazli za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Wamiliki na Madereva watakaoruhusu magari kutumika yakiwa mabovu.
Kamanda Ng’azi ametoa marufuku hiyo wakati akiwa katika ziara ya kikazi Wilayani Masasi Mkoani Mtwara, wakati akikagua mabasi 15 ambapo kati ya hayo basi moja lilibainika kuwa ni bovu na halifai kuendelea na safari, kutokana na hitilafu kwenye mfumo wa breki.
Amesema, “nasikitishwa sana na kuumizwa sana na ajali za barabarani zinapotokea na kupelekea vifo, majeruhi na uharibifu wa miundombinu. Pia sifurahishwi kuona madereva wanaendelea kuendesha magari yao yakiwa hayajakaguliwa na wakati wanao mafundi wao binafsi.”
Hata hivyo, amesema Jeshi la polisi litafanya ukaguzi wa kina ili kuyabaini magari mabovu na kutoyaruhusu kufanya shughuli za usafiri na usafishaji, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mmiliki na dereva yeyote atakaeruhusu gari lake kutumika barabarani likiwa bovu.