Tangu ukoloni na hata baada ya Taifa la Tanzania kupata uhuru wake mwaka 1961, Wizara ya Ulinzi haikuwahi kushikwa au kuongozwa na Mwanamke, kiasi ilikwisha kuzoeleka au kujengeka vichwani mwa watu kuwa Wizara hiyo ni kwa upande wa jinsia ya kiume pekee, jambo ambalo halikuwa na sahihi kimtazamo.
Lakini rekodi hii ikavunjwa rasmi, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kumteuwa Dkt. Stergomena Tax kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kumaliza muda wake akiwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika – SADC.
Septemba, 2021 Rais Samia akafanya mabadiliko madogo katika baraza lake la Mawaziri na miongoni mwa sura mpya katika baraza hilo akaonekana mbunge huyo wa kuteuliwa Dkt. Tax, ambaye akawa Mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania na hivyo kubadili mtizamo wa kila aliyedhani Wizara hiyo ni kwa Wanaume pekee.
Mara baada ya kuwaapisha Mawaziri aliowateua, Rais Dkt. Samia alizungumzia mambo mengi ya kiutendaji, na miongoni mwa hayo pia aligusia uteuzi wa Dkt. Tax akisema aliamua kuvunja mwiko na fikra zilizojengeka kuwa Wizara ya Ulinzi na JKT, lazima iongozwe na Mwanaume kwani Waziri haendi kule ili kupiga mizinga wala kubeba bunduki, bali Waziri anawajibika.
“Nimeamua kuvunja mwiko wa muda mrefu kwamba Wizara ya Ulinzi lazima akae Mwanamme mwenye misuli yake, lakini kazi ya Waziri kwenye Wizara ile si kupiga Mizinga wala kubeba Bunduki, ni kusimamia sera na utawala wa Wizara, nikaamua Dada yetu Stergomena Tax nimpeleke huko, sijampeleka sababu tu ya kuvunja mila lakini ni kwa upeo wake mkubwa alioupata akiwa SADC,” alisema.
Baadaye Oktoba 2, 2022 Rais Samia akafanya tena mabadiliko ya Wizara na kuhamishia Dkt. Tax Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Nafasi yake ikashikwa na Innocent Bashungwa aliyehamishwa Wizara, akitokea Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Mengi yaliongelewa, lakini majibu yakafuata baada ya Rais Samia kuonesha kuwa hakukosea kwani Agosti 30, 2023 Rais Samia akaona kuna haja ya kufanya mabadiliko katika Serikali yake ili kuimarisha na kuboresha utendaji, hapo Dkt. Stergomena Tax akarejeshwa tena kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, akitokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ninachotaka kusema ni kuwa, fikra zako hujenga hisia zako kuliko uhalisia wa matukio yenyewe, kwa mfano ukifikiria watu au vitu kwa mabaya, basi utaona mabaya pekee na ukitazama mazuri ya watu au vitu utaona pia mambo mazuri ila kumbuka hakuna kitu kizuri au kibaya kinachokuwa na asilimia 100.
Ipo hivyo pia katika fikra zetu kwani wakati mwingine tunaamini kuwa jambo fulani ni kwa ajili ya watu fulani pekee, hiyo si sahihi hata kidogo kwani waweza jikuta unapishana na ukweli au mtu kushindwa kukuelimisha jambo kutokana na misimamo, hivyo tupende kujifunza zaidi na kutanua mawazo yetu kwamba Dunia ya sasa inahitaji ushirikiano na ushirikiano huleta mafanikio na kujenga tabia mpya, MAMA KABADILI FIKRA MAMA KATOA SOMO.