Lydia Mollel – Morogoro.
Wakati Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, likiendelea kutoa elimu na kufanya doria katika maeneo mbalimbali, pia limefanikiwa kumkamata Mwananchi mmoja Mkude Berege (42), mkazi wa Kitongoji cha Kwiro Kata ya Dogomajiji Wilayani Malinyi, kwa kosa la kuwabeba watoto watano wa familia yake kwenye pikipiki moja.
Akizungumza na Mwananchi huyo Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Shangwe Mlela amesema ubebaji huo ni hatari na unaweza kusababisha madhara makubwa pindi itakapotokea ajali, hivyo kuampa onyo juu ya kitendo hicho.
Amesema, “sheria hairuhusu ubebaji wa aina hii lakini pia hawa ni watoto uwezo wao wa kijishikilia ni mdogo unaweza ukashajikuta umewaacha njiani.”
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Mwaipopo ambaye aliambatana na ASP Mlela katika utoaji wa elimu hiyo amesema, aina hiyo ya uvunjifu wa sheria umekuwa mazoea kwa wakazi wa Kijiji hicho, jambo ambalo limepelekea kuona uhitaji wa kutoa elimu au kuchukua hatua ili kuepusha madhara.
Hata hivyo, watumiaji wa vyombo vya moto pia wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani kwa usalama wao, abiria, na watumiaji wengine wa barabara ili kuepukana na ajali.