Wanaume wametakiwa kuwasindikiza wenza wao wakati wa ujauzito, ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo upimaji wa Virusi vya UKIMWI na maambukizi ya Kaswende.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Mkoa wa Iringa, Wende Mwavika ambaye ameongeza kuwa ushiriki wa Wanaume katika masuala ya upimaji umekuwa ni mdogo, jambo linalopelekea kutofikia lengo la upimaji wa maambukizi ya Kaswende.
Amesema, Wanawake wajawazito wamekuwa wakijitokeza kupata vipimo bila wenza wao na kudai kuwa ni muhimu wenza kupata matibabu ya pamoja wanapobainika kuambukizwa, hali itakayosaidia kupunguza maambukizi ya Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Kaswende, ukifahamika kama “syphilis” kwa Kiingereza ni ugonjwa wa maambukizi ya bakteria kwa njia ya kujamiiana (STD) na dalili za awali ni vidonda vidogo kwenye sehemu za siri na tezi za limfu kuvimba, ambao huathiri sehemu tofauti za mwili na inaarifiwa kuwa utumiaji wa kinga wakati wa kujamiiana huweza kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa huo.