Mshambuliaji tegemeo wa Namungo FC, Reliants Lusajo, ametangaza kuachana timu hiyo na kusema anahitaji kwenda kupata changamoto mpya.
Ingawa hajaweka wazi wapi anakwenda, taarifa zilizopatikana zinasema straika huyo anawindwa na Singida Fountain Gate FC pamoja na Azam, katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Timu hizo mbili zinatajwa kuhitaji huduma ya Lusajo katika mipango ya kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.
Joshua Kimmich ageuka lulu England
“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Namungo FC na Benchi la Ufundi bila kusahau Mashabiki wote wa timu hiyo kwa kipindi chote tulichokua pamoja, ni muda wangu sasa wa kuangalia changamoto sehemu nyingine, nipende kuwatakia kila la kheri katika msimu huu wa ligi.” amesema mchezaji huyo ambaye amefunga mabao mawili msimu huu.
Hata hivyo viongozi wa Namungo FC bado hawajasema lolote kuhusu uamuzi wa mshambuliaji huyo ambaye anatajwa amemaliza mkataba na timu hiyo ya mkoani Lindi.
Lusajo ambaye aliwahi kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ni mmoja wa mastraika wachache Watanzania ambao wana uwezo wa kupachika mabao angalau 10 kwa nsimu mmoja, alianza kujulikana akiwa na kikosi hicho tangu mwaka 2020.
Nyota huyo pia aliwahi kuitumikia KMC, lakini akarejea tena Namungo FC katika mzunguko wa pili wa msimu wa 2020/21 hadi jana alipotangaza kuachana na timu hiyo.