Beki kutokla nchini Ufaransa na Klabu ya Arsenal, William Saliba amekuwa gumzo mtandaoni baada ya kukiri Liverpool ilistahili Penati kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu England uliofanyika Jumamosi (Desemba 23).

Arsenal na Liverpool ilifungana 1-1 uwanjani Anfield kwenye kipute cha Ligi Kuu England.

The Gunners ilitangulia kufunga kupitia kwa beki Gabriel Magalhaes katika dakika ya nne tu ya mchezo, lakini Liverpool ilisawazisha kupitia staa wao Mohamed Salah dakika 25 baadae.

Hata hivyo, Liverpool inadhani ilistahili kuzoa pointi zote tatu kama wasingenyimwa Penati yao kwenye kipindi cha kwanza kabla ya Mo Salah kufunga bao la kusawazisha.

Mo Salah alikokota mpira kumpita Martin Odegaard, ambaye aliteleza na kuugusa mpira kwa mkono wake wa kushoto ndani ya boksi la goli la Arsenal.

Hata hivyo, mwamuzi aliamuru mechi iendelee na VAR wala haikuhusishwa jambo lililowafanya mashabiki wa timu mwenyeji kukasirika.

Na Saliba, ambaye alicheza kwa kiwango matata kabisa katika mechi hiyo, aliulizwa kuhusu kitendo hicho cha Odegaard.

Beki huyo alikiri nahodha wa Arsenal alishika mpira na Liverpool ilistahili penalti, akisema: “Yeah, bila shaka ile ni penalti, lakini mimi sio refa.”

Maneno ya beki huyo Mfaransa amekuwa maarufu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana kuwa ni kitu tofauti sana kwa mchezaji wa timu pinzani kukiri penalti ya timu nyingine.

Gwiji wa Liverpool, Jamie Carragher alimsifu Saliba mwenye umri wa miaka 22 na kuishambulia VAR.

Kocha Azam FC aihofia Young Africans Ligi Kuu
Kauli ya Lusajo yaibua minong'ono