Mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Enock Atta Agyei ameibua madai kuwa ametelekezwa tangu alipoumia miezi mitano iliyopita, huku akisisitiza kutolipwa mshahara kwa miezi mitatu.
Hata hivyo, msemaji wa timu hiyo, Hussein Massanza alipoulizwa juu ya madai hayo amesema hana taarifa na kwamba anachojua mchezaji huyo ni majeruhi na yupo nje ya timu akiuguza majeraha.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo ambaye alijiunga na Singida Fountain Gate kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Horoya AC ya Guinea mwanzoni mwa msimu huu, amesema kwamba amekuwa akijaribu kuwapigia viongozi kujua hatima yake, lakini hapati ushirikiano unaotakiwa.
“Nimekuwa majeruhi kwa miezi mitano. Timu hainijali nipo tu nyumbani na jitihada zangu za kupiga simu na kutuma meseji hazinisaidii, kwani sijibiwi na hata simu ikipokewa wamekuwa wakiishia kunidanganya hakuna wanachofanya kwa ajili yangu,” amesema.
“Bado nina mkataba wa miaka miwili na nusu. Walimpigia simu wakala wangu wanataka kuachana na mimi sababu sina nachofanya ndani ya timu ilhali niliumia nikiwa kikosini.”
Mchezaji huyo amesema baada ya uamuzi huo alikubaliana na wakala wake kuwa yupo tayari kuachwa, lakini anatakiwa kulipwa fedha zake.