Timu za Mashujaa FC na Mtibwa Sugar ambazo zinashika nafasi mbili za mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara zinadaiwa kusaka saini ya Mlinda lango wa Simba SC, Hussein Abel katika Dirisha Dogo la usajili linaloendelea kwa sasa.

Mashujaa inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara huku Mtibwa Sugar ikiburuza mkia kati ya timu 16 zinazoshiriki michuano hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa, wakati Mashujaa FC inafukuzia kumsajili Abel, Mtibwa imeshatuma barua Simba SC ikimtaka Mlinda Lango huyo kwa mkopo. Hata hivyo, timu hiyo bado haijajibiwa.

Kwa upande wa Mashujaa FC, Kocha Mohamed Abdallah Baresi ameamua kusuka upya kikosi chake kilichopanda Ligi Kuu Bara msimu huu 2023/24.

Abel alisajiliwa na Simba SC msimu huu akitokea KMC na katika mechi 10 za ligi ambazo imecheza ni dhidi ya KMC pekee iliyotoka sare ya mabao 2-2 ndio alikaa benchi.

Nyota huyo amekuwa na wakati mgumu ndani ya Simba SC kutokana na ushindani uliopo kutoka kwa makipa wenzake Ayuob Lakred ambaye sasa anaaminiwa kukaa langoni, Ally Salim huku Aishi Manula aliyekuwa namba moja yupo nje ya uwanja baada ya kujitonesha jeraha.

Hata hivyo, Manula ameitwa kwenye kikosi kinachojiandaa na Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zinazotarajia kuanza Januari 13, 2024 nchini Ivory Coast.

Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya Simba SC zinaeleza kuwa, huenda kukawa na ugumu kumwachia Abel wakati hakuna uhakika juu ya Manula ambaye awali ilielezwa atarejea uwanjani Februari 2024, hivyo ndani ya kikosi kubaki na makipa watatu wa uhakika ukiachana na Ahmed Ferouz ambaye alipandishwa kutoka U20.

Alipotafutwa kuzungumzia suala la usajili, Baresi amesema: Nimewapa ripoti mabosi wangu, hivyo natarajia itafanyiwa kazi ili tuwe na kikosi imara zaidi. Nani namhitaji? Basi ni suala la muda utakapofika wa kukamilisha kila kitu.”

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Desemba 27, 2023
Coastal Union kusajili Kenya, Uganda