Klabu ya Azam FC imetamba kuendeleza kasi yake ya ushindi katika Ligi Kuu Tanzania Bara, pindi itakaporejea baada ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazounguruma nchini Ivory Coast kuanzia Januari 13, 2024.

Tambo hizo za Azam FC zimekuja kufuatia kasi ya ushindi waliyonayokatika Ligi Kuu, na sasa wameelekea katika Mshike Mshike wa Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, itakayofanyika Kisiwani Unguja, Zanzibar.

Timu hiyo inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 31 katika mechi 13, hivi karibuni imekuwa ikionyesha ubora wa hali ya juu na kufanikiwa kushinda mechi sita mfululizo.

Katika mechi hizo, Azam FC ilianza kwa kuifunga Mashujaa FC mabao 3-0, Ihefu (3-1), Mtibwa (5-0), KMC (5-0), JKT Tanzania (2-1) kabla ya Alhamisi ilyopita kuipasua Kagera Sugar mabao 4-0.

Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem lbwe, amesema kikosi chao kimepanga kuendeleza makali yake ligi itakapoendelea mwaka 2024.

“Kila mchezaji anatambua tunahitaji nini, tutaendelea kupambana kupata matokeo chanya tuweze kufikia malengo yetu tuliojiwekea msimu huu wa 2023/24,” amesema

Amesema pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa na ushindani mgumu, lakini ana imani wachezaji wao wataendelea kufanya vyema kupata ushindi katika mechi zao.

Tayari kikosi cha Azam FC kimeshaelekea Kisiwani Unguja, Zanzibar kwa ajili ya Michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza kesho Alhamis (Desemba 28) katika Uwanja wa Amaan.

Katika michuano hiyo, Azam FC ipo kundi A na timu za Chipukizi, Mlandege (Zanzibar) na Vital’O ya Burundi.

Azam FC itafungua michuano hiyo kwa mchezo dhidi ya Mlandege utakaopigwa kesho saa 10:15 jioni.

Benchikha kunoa makali Mapinduzi CUP
Rais Mwinyi mgeni rasmi Kili Stars Vs ZNZ Heroes