Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wameingia kambini leo Jumanne (Desemba 27) kuanza kujiwinda na mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Jamhuri utakaochezwa kwenye Uwanja Amaan, Zanzibar Jumapili (Desemba 31).

Young Africans imepangwa Kundi C na timu za Jamhuri na KVZ zote kutoka visiwani Zanzibar na Jamus kutoka Sudan Kusini.

Michezo yote ya Kombe la Mapinduzi itachezwa katika Uwanja wa Amaan na kesho Alhamis (Desemba 28) ndio ufunguzi kati ya Mandege dhidi Azam FC saa 10-00 jioni.

Ofisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe, amesema kuwa baada ya mapumziko mafupi waliyopewa wachezaji baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tabora United wamerudi kuanza kujiwinda na Kombe la Mapinduzi.

“Kikosi kimerejea kambini leo kuaza kujiwinda na michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo ni mashindano muhimu kwetu kutengeneza muunganiko wa kikosi chetu.

Lakini pia ni wakati wa kwenda kutambulisha nyota wapya tuliowasajili kwenye dirisha dogo la usajili na kwenye mhezo wetu wa kwanza tutatambulisha kifaa chetu kipya ambacho  kimekuja kuongeza nguvu kikosini,” amesema Kamwe.

Katika hatua nyingine Kamwe amesema kikosi cha Young Africans kinatarajia kuanza safari kesho Alhamis (Desemba 28)  kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano hiyo ambayo malengo yao ni kuhakikisha wanarudi nyumbani na kombe.

Mchezo wa pili Young Africans itacheza na Jamus FC, Januari 2 mwakani na mchezo wa mwisho kwenye makundi watacheza na KVZ Januari 4.

Maxime afunguka killichomng’oa Kagera Sugar
Makala: Ukweli kuhusu ujenzi wa Hotel kwenye Sayari ya Mars