Wakati Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC ililyoko chini ya Mwenyekiti, Salim Abdallah (Try Again) imepokea ripoti rasmi ya mapendekezo ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa katika kipindi cha dirisha dogo, klabu hiyo imetamba inakwenda kuwapa furaha Mashabiki na Wanachama wake katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi.
Ripoti ya benchi la ufundi imeweka wazi inahitaji kusajili wa wachezaji wapya kati ya watano na sita ili kuimarisha kikosi chao kinachowania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kinashiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nyota wapya wanaotakiwa Simba SC ni wa nafasi ya kiungo mkabaji, beki wa kati na mshambuliaji.
Taarifa zilizopatikana jijini Dar es salaam zinasema tayari Wekundu wa Msimbazi wamemnasa Kiungo Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Ladack Chasambi, na kumpa mkataba wa miaka mitatu.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema tayari Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, amekabidhi ripoti yake ambayo imeainisha maeneo anayotaka kuboresha katika kikosi chake.
“Viongozi wamepokea mapendekezo hayo na kuanza kuyafanyia kazi, ni kweli tunahitaji wachezaji kuimarisha kikosi chetu, tuliokuwa nao si wabaya bali wanahitaji kujituma na kujitoa kitu ambacho tunakikosa katika timu yetu.
Tunatarajia kuongeza mashine ambazo zitakuja kusaidiana na hawa waliopo, kama tutafanikiwa kukamilisha usajili wa nyota wapya mapema wataungana na timu Visiwani Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi,” amesema ofisa huyo.
Kuhusu maandalizi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi amesema kikosi chao kinaingia kambini leo Jumatano (Desemba 27) na kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena kwa ajili ya kujiweka tayari na mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka.
“Kikosi kinatarajia kuondoka Desemba 30 au 31, mwaka huu kuelekea Zanzibar, na tayari kwa mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Jamhuri utakaochezwa Januari Mosi, 2024.
Tutatumia mashindano hayo kujiweka imara na kocha (Benchikha) atapata muda mzuri wa kufanya mazoezi na kukaa na wachezaji wake kuona uwezo wa mmoja mmoja mbali na wale waliokuwa katika majukumu ya timu za Taifa,” amesema meneja huyo.
Ameongeza hakuna mchezaji majeruhi mpya zaidi ya Aubin Kramo ambaye yuko katika hatua ya mwisho za matibabu yake baada ya kukaa nje kwa muda mrefu.
“Phiri (Moses), ameingia katika siasa ambazo kiungo wetu Clatous Chama aliwahi kuingia katika miaka ya hivi karibuni ya kuhusishwa kutakiwa na klabu moja ya hapa nchini lakini kwa miaka yote anaitumikia Simba SC.
Phiri bado ana mkataba na Simba SC, hatujapokea barua yoyote kutoka kwa nyota huyo, kama anahitaji kuondoka atalazimika kufuata taratibu,” amesema Ahmed Ally.
Ameongeza licha ya Chama kusimamishwa, lakini kiungo huyo anaendelea na programu za mazoezi aliyopewa na Benchi la Ufundi pamoja na kulipwa stahiki zake ikiwamo mshahara wake.