Klabu ya Azam FC inatajwa iko katika mazungumo ya kumsajili Mlinda Lango wa Tanzania Prisons Yona Amosi, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi chao kwenye dirisha dogo la Usajili.

Taarifa za ndani zinasema Yona amekuwa akihusishwa na Azam FC tangu msimu uliopita kwa ajili ya kuchukua nafasi ya makipa waliopo, Abdulah Iddrisu na Ali Ahamada.

Hata hivyo pia Metacha Mnata na Abdultwalib Mshery, wote kutoka Young Africans pia wanatajwa kuwa katika mazungumzo ya kujiunga na klabu hiyo tajiri hapa nchini.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino Azam FC, Thabiti Zakaria (Zaka), amesema wataongeza ‘mtu hasa’ katika nafasi ya kipa kwa sababu walinda mlango waliopo ni majeruhi na watakaa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Zaka amesema wako makini katika usajili watakaofanya na wanaamini watapata kipa mzuri na bora atakayeenda kusaidia kikosi chao ambaye huenda akatoka ndani au kutoka nje ya nchi.

“Tutaongeza wachezaji, kipaumbele chetu ni Mlinda Lango kwa sababu tuliokuwa nao ni majeruhi wa muda mrefu, kipa wa kigeni si kipaumbele chetu bali tunahitaji nyanda mzuri kuja kusaidiana na makipa wetu kutoka timu ya vijana.

Kuhusu Mlinda Lango wa Tabora United, John Noble, ni mkubwa sana na namhusudu sana. Lakini hayuko kwenye mipango yetu, na nyanda tutakaemsajili tutanuniwa na watu,” amesema Zaka.

Kuhusu maandalizi kuelekea mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Zaka amesema kikosi chao kimeondoka jijini, Dar es salaam leo Jumatano (Desemba 27) kuelekea Zanzibar tayari kwenda kupambana kuwania taji hilo.

Azam FC watashuka dimbani kesho Alhamis (Desemba 28) kuvaana na mabingwa watetezi Mlandege FC, mechi itakayochezwa kuanzia saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa Amaan.

Steven Gerrard hali mbaya Saudi Arabia
Zaidi ya Kilo 3,000 za dawa za kulevya zakamatwa Dar, Iringa