Uongozi wa Mtibwa Sugar umeahidi kufanya usajili kwa mujibu wa Ripoti ya Benchi la Ufundi, ili kuinusuru timu yao na janga la kushuka daraja.

Ahadi hiyo kutoka kwa viongozi wa Mtibwa Sugar imekuja wakati muafaka, huku ukisisitiza kusajili wachezaji wenye uzoefu katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 15.

Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, amesema licha ya dirisha dogo la usajili kutotakiwa kusajili idadi kubwa ya wachezaji, timu yao italazimika kufanya hivyo ili kujiweka katika nafasi salama.

“Tumepokea ripoti ya mwalimu wetu, ameweka wazi maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi, ametaka eneo la golikipa asajiliwe mwingine, maboresho mengine ni eneo la mlinzi, viungo na washambuliaji,”

“Ripoti imesema wanaotakiwa kusajiliwa ni wachezaji bora, wenye uwezo na wazoefu wa ligi, utaona hapo ni usajili mkubwa unatakiwa kufanyika, viongozi wamepokea na watalifanyia kazi, lengo ni kuhakikisha timu haishuki daraja, Mtibwa Sugar ni timu kubwa yenye heshima nchini, ukiondoa Simba SC na Young Africans,” amesema Kifaru.

Mtibwa Sugar inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imesalia raundi moja tu kumaliza mzunguko wa kwanza, ligi hiyo imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi na Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’.

Msuva azikataa Young Africans, Simba SC
Onana atahadharishwa Manchester United