Mshambuliaji wa Mbuni FC, Salim Aiyee yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha dili la usajili la kujiunga na Coastal Union katika dirisha hili dogo la usajili ikiwa ni pendekezo la kwanza kwa kocha mkuu wa timu hiyo Mkenya, David Ouma.

Dirisha la usajili lilifunguliwa Desemba 15 na linatarajiwa kufungwa Januari 15 mwakani, huku Wagosi wakiwa wameshatangaza kuachana na wachezaji wawili, Mapinduzi Balama na beki Mcroatia, Fran Golubic.

Ofisa Habari wa Coastal, Abbas Elsabri amesema kuwa, tayari mazungumzo na baadhi ya wachezaji wapya watakaowasajili yameshaanza rasmi na muda wowote kuanzia sasa wataweka wazi majina ya wale waliofikia makubaliano.

“Kwa sasa ni mapema sana kuzungumzia suala la Aiyee lakini kama litakuwepo tutawafahamisha mashabiki wetu, malengo yetu ni kufanya vizuri msimu huu hivyo tutasajili kwa matakwa ya benchi la ufundi na sio kusajili tu.” amesema Elsabri.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Mbuni, Leonard Budeba amesema ni kweli nyota huyo yupo kwenye mazungumzo na Coastal Union ingawa bado makubaliano binafsi hayajafikiwa, huku akieleza ni pigo kubwa kwao endapo itamkosa mshambuliaji huyo kinara.

Akiwa na Mbuni msimu huu nyota huyo tayari amefunga mabao tisa katika michezo 14 aliyocheza akipitwa mawili tu na vinara Edgar William wa KenGold na Mganda Boban Zirintusa ambaye anaichezea Biashara United ambao kila mmoja wao amefunga 11.

Aiyee aliyechezea Geita Gold na KMC anakumbukwa zaidi wakati akiwa Mwadui FC msimu wa 2018/2019 ambapo alifunga jumla Va mabao l8 nyuma ya nyota Wa zamani wa Simba, Meddie Kagere anayekipiga Singida Fountain Gate kwa sasa ambaye alifunga 23.

Alcantara kuondoka Liverpool
Seif Karihe akataa kukaa kizembe