Matumizi ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia wa baadhi ya watu katika jamii, vimetajwa kuwa ni sababu mojawapo inayopelekea wao kujiingiza kwenye utendaji wa matukio ya kiuhalifu.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi George Katabazi wakati akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake.
Amesema, “jamii tushirikiane kukemea matumizi ya dawa za kulevya kwani vijana wengi wakishatumia hujiingiza katika kufanya uhalifu hususani ukatili wa Kijinsia.”
Aidha, Kamanda Katabazi ameeleza kuwa Doria na Operesheni za kuwakamata watuhumiwa wa dawa za kulevya hasa Bangi, mirungi na Pombe Moshi maarufa kama Gongo bado zinaendelea maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na kuwataka wahusika kuacha mara moja.
Hata hivyo, amesema kwa kushirikiana na vikundi vya Ulinzi pamoja na Jamii watazidisha vita na kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya pamoja na pombe haramu ya Moshi katika kukabiliana na uhalifu na wahalifu Mkoani humo.