Beki wa kati wa Simba SC, Henock Inonga na Mshambuliaji wa zamani wa Young Africans ambaye kwa sasa anakipiga klabu ya Pyramid ya Misri, Fiston Mayele wamepenya kwenye kikosi cha wachezaji 24 wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kikosi hicho ndicho kitakachoshiriki Fainali za Mataifa ya Africa ‘AFCON 2023’, zitakazofanyika nchini Ivory Coast kuanzia Januari 13 mwakani.

Nyota hao walijumuishwa kwenye kikosi cha awali kilichokuwa na jumla ya wachezaji 45 kabla ya kuchujwa na kocha wa timu hiyo Sebastian Desabre na kubaki wachezaji 24 watakaoipeperusha bendera ya nchi hiyo kwenye Fainali hizo.

Inonga aliitwa kwenye timu hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2022 alipojiunga na Simba SC na tangu wakati huo amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha timu hiyo kwenye mashindano ya kuwania kufuzu kwa Fainali hizo na Kombe la Dunia.

Inonga pia anakuwa mchezaji pekee kutoka DRC wanaocheza Ligi Kuu Soka Tanzania Bara kuitwa kwenye timu hiyo kwa ajili ya Fainali hizo huku nyota wengine kama Max Nzengeli, Jesus Moloko, Joyce Lomalisa kutoka Young Africans na Jean Baleke wa Simba SC hawakuwemo hata kwenye orodha ya awali iliyotajwa kocha Desabre.

Kikosi hicho cha Kocha Sebastian Desabre kinaundwa na Walinda lango Lionel Mpasi (Rodez, Ufaransa), B Ngusia Siadi (TP Mazembe) na Dimitry Bertaud (Montpellier, Ufaransa).

Mabeki ni Brian Bayeye (Ascoli, Italia), Rocky Bushiri (Hibernians, Scotland), Gedeon Kalulu (Lorient, Ufaransa), Dylan Batubinsika, Arthur Masuaku (Besiklas, Uturuki) Chancel Mbemba (Olimpique Marseille, Ufaransa) na Joeis Kayembe (Genk, Ubelgiji).

Viungo ni Edo Kayembe (Watford, Uingereza), Silas Katompa (Stuttgart, Ujerumani), Charles Pickel (Cremonese,Italia), Meshack Elia (Young Boys, Uswisi), Samuel Mouttoussamy (Nantes, Ufaransa), Theo Bongonda (Spartak Moscow, Urusi),Aaron Tshibola(Hatta, Uarabuni), Glady Diangana (West Bromwich Albion, Uingereza) na Gael Kakuta (Amiens, Ufaransa).

Washambuliaji ni Yoane Wissa (Brentford, Uingereza), Cedric Bakambu (Galatasaray, Uturuki), Simon Banza (Sporting Braga, Ureno) na Fiston Mayele (Pyramids, Misri).

Man City kufungua pochi kwa Echeverri
Dawa za kulevya, ulevi kupindukia chanzo matukio ya uhalifu