Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amesema mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwake ni muhimu katika kukijenga kikosi chake kabla ya kurejea kwenye michuano ya Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.
Benchikha amesema atayatumia mashindano hayo kuwapa mbinu wachezaji wake.
“Hii ni nafasi nzuri kwetu kuiandaa timu yetu, wiki mbili za mashindano haya zitanipa nafasi kubwa ya kuandaa timu na kuiboresha zaidi,” amesema Benchikha.
Aidha, kocha huyo ametaka Uongozi wa klabu hiyo kufanya usajili kwa kuboresha baadhi ya maeneo huku ikielezwa kutaka kusajiliwa beki wa pembeni kwa ajili ya kumpa changamoto nahodha msaidizi, Mohamed Hussein Tshabalala’
Inaelezwa awali Simba SC walikuwa na nia ya kumsajili beki wa pembeni wa Mamelod Sundown, Aubrey Modiba mwenye Umri wa miaka 28 lakini dili hilo limekufa.
Simba SC kwa sasa wamemgeukia beki wa CSMD ya Congo Brazaville, Hernest Briyock Malonga ambaye wameanza mazungumzo ya kumsajili.
Habari zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi vinasema Simba SC imepeleka ofa kwa kutaka kumnasa beki huyo wa kushoto, huku ikimpiga chini lbrahim Imoro aliyemaliza mkataba na Al Hilal ya Sudan kwa madai kwa sasa klabu hiyo haihitaji kumsajili mchezaji huru.
“Mpango wa kumsajili Modiba haupo, kwa sababu hakuna mazungumzo baina ya Simba SC na Mamelodi Sundowns kuhusu Usajili wa mchezaji huyo, lakini klabu imepeleka ofa kwenye klabu ya CSMD Diables Noirs kwa ajili ya kumsajili beki wao Malonga mwenye miaka 21 na huyo ndiyo wanayemtaka sasa.
“Kuna mchezaji anaitwa Imoro wa Al Hilal ambaye amemaliza mkataba wake kwenye klabu hiyo, kuna mawakala walipeleka jina lake ili asajiliwe, lakini Uongozi wa Simba SC wamemkataa kwa kuwa hawataki kusajili mchezaji huru na hata Kocha Benchikha ajaafikiana na mchezaji huyo,” amesema mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.
Kikosi cha Simba SC kimeanza mazoezi jana Jumatano (Desemba 27) kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena baada ya mapumziko ya Sikukuu ya Krisimasi kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la Mapinduzi, linalotarajiwa kuanza leo Alhamis (Desemba 28) mjini Zanzibar.
Simba ipo Kundi B na inatarajiwa kuingia dimbani mwaka mpya, Januari Mosi kucheza dhidi ya JKU katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kwenye michuano hiyo.