Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Saidi Mabie amewataka Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Stadi vilivyopitishwa na Serikali, kutoa mafunzo ya Uanagenzi kuhakikisha vitendea kazi na malighafi za kufundishia zinapatikana kwa wakati, ili Vijana wajifunze kwa vitendo.
Mabie ameyasema hayo Jijini Dodoma katika kikao cha kusaini hati za makubaliano za kutoa mafunzo ya uanagenzi awamu ya sita, kwa Wanafunzi 6000 wanaotarajiwa kuanza mafunzo hayo Januari 2024.
Amesema, uwepo wa vitendea kazi unarahisisha uelewa, pia kuleta mchango mkubwa katika kuboresha kiwango cha ujuzi katika soko la Ajira na kuwezesha azma ya serikali ya kuwa na vijana wenye kuajirika ama kujiajiri wenyewe.
“Tutapita kufuatilia utekelezaji wa mafunzo husika pamoja na viongozi wetu na mfahamu kwamba utekelezaji wa mafunzo haya utakuwa sambamba na ufuatiliaji wa mara kwa mara na kwa kina,” alisema Mabie.