Wakati Fainali za Mataifa ya Bara la Afrika ‘AFCON 2023’ zikikaribia kuanza, idadi kubwa ya timu zinazoshiriki fainali hizo zimepanga kucheza michezo ya Kimataifa ya Kirafiki, kama sehemu ya maandalizi ya michuano hiyo ambayo itaanza Januari 13, 2024 nchini Ivory Coast.
Mechi tisa za kirafiki zimethibitishwa na timu zinazoelekea kwenye ‘AFCON 2023’ kwa ajili ya michuano hiyo itakayoshirikisha mataifa 24 itakayoendelea hadi Februari 11 huko Afrika Magharibi.
Kama sehemu ya maandalizi yao, mabingwa mara tatu wa Afrika, Nigeria wamepanga kucheza mechi mbili za kirafiki.
Nigeria Super Eagles’ itakabiliana na Leopards ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Stalions ya Burkina Faso.
Mabingwa mara nne wa Afrika, Ghana “Black Stars’ wamepanga mechi ya kirafiki dhidi ya Botswana.
Mabingwa wa kihistoria, Misri watakutana na Tanzania katika mechi nyingine ya kirafiki wakati pande zote mbili zikijiandaa kwa hatua ngumu ya makundi.
Burkina Faso pia itakutana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakati washindi mara tano, Cameroon wakifunga pembe na washindi wa 2012 Chipolopolo wa Zambia huko Jeddah.
Mabingwa watetezi, Senegal wana miadi dhidi ya Menas ya Niger Januari 7 katika Uwanja wa Abdoulaye Wade huko Dakar. Angola na Guinea Bissau pia wamepanga kujipima kabla ya AFCON.