Mabingwa wa Soka Tanzania Bara ‘Young Africans’ wamesema wanapeleka kikosi chao chote visiwani Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyoanza jana Alhamis (Desemba 28) huku pia ikikanusha taarifa zilizoenea kuwa itakwenda na kikosi cha pili.
Pia uongozİ wa klabu hiyo umeweka wazi haina mpango wa kumsajili mshambuliaji Sankara Karamoko kutoka Asec Mimosas katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe amesema, Kocha Mkuu, Miguel Garmondi amewaambia wachezaji wake wote kuwa yeyote ambaye hajachaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa na si majeruhi, basi ana wajibu wa kuambatana na kikosi hicho mjini Zanzibar.
“Tunapeleka kikosi chetu chote Zanzibar, isipokuwa wale ambao wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa na wale majeruhi tu, wote waliokuwa fiti watakwenda kucheza Kombe la Mapinduzi, kocha Gamondi amewaambia wachezaji kuwa hatokubali udhuru wowote wa mchezaji ambao utamkosesha kwenda huko,” amesema Kamwe.
Kauli hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa tetesi kuwa Young Africans ingepeleka kikosi cha wachezaji ambao hawapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza huku mastaa wake wakitajwa kwenda mapumziko mafupi baada ya ligi kusimama.
“Lazima twende kamili ili tukawape furaha mashabiki wa Young Africans Zanzibar, kwa hiyo nawaambia wote watakuwepo hadi Skudu (Mahlatse Makudubela) atakuwepo.
Young Africans itaanza mechi ya kwanza ya michuano hiyo keshokutwa Jumapili (Desemba 31), itakapocheza dhidi ya Jamhuri.
Kamwe amesisitiza kuwa siku hiyo klabu itamtambulisha mchezaji mpya kama ambavyo wameshatangaza awali.
Hatujabadilisha, siku hiyo pia kuna sapraizi, tunatarajia kutambulisha mchezaji wetu mpya kama ambavyo tumeshasema na tunarudia ni mchezaji ambaye wengi wanamfahamu,” amesema Kamwe.