Endapo mambo yatakwenda kama yalivyopangwa, huenda Jumanne (Januari Pili) Klabu ya Simba SC ikampokea winga Mauricio Cortes Nunez mwenye umri wa miaka 26 raia wa Colombia kwa ajili ya kukamilisha taratibu za mwisho za usajili, huku klabu hiyo ikikiri kuwa inafanya usajili wa nguvu ambao itautangaza baadae.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa klabu hiyo juu ya usajili kwenye dirisha hili dogo.
“Watu wanaendelea kusajiliwa huko nyuma ya pazia, ni usajili wenye tija kwa klabu yetu, mashabiki na wanachama watulie mambo yatakapokamilika tutawatangazia kila kitu.” amesema Ahmed.
Ingawa hakutaja majina ya wachezaji ambao inawasajili, lakini taarifa za ndani ya klabu hiyo, zinasema tayari imempata winga huyo wa Colombia akitokea kwenye klabu ya Commerciantes huku ikielezwa kuwa atapewa mkataba wa miaka miwili.
Wachezaji wengine wanaohusishwa kujiunga na timu hiyo ni beki wa kushoto Hernest Briyock Malonga anayeichezea klabu ya CSMD Diables Noirs ya Congo Brazaville kiungo mshambuliaji Miche Mika wa FC Saint Eloi Lupopo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kiungo mkabaji Erick Mbangossoum raia wa Chad anayeichezea klabu ya Union Touarga ya nchini Morocco.
Kwa upande wa wachezaji wa Kitanzania, taarifa zinasema klabu hiyo tayari imekamilisha usajili wa Ladack Chasambi ya winga anayecheza nafasi na kiungo mshambuliaji kutoka Mtibwa Sugar.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Thobias Kifaru ameserma wameshamalizana naye na kumruhusu kwa baraka zote, huku pia Wekundu wa Msimbazi wakiwa kwenye mazungumzo na wachezaji wengine, Edwin Barua wa Prisons anayecheza nafasi ya pembeni na mshambuliaji wa Geita Gold Valentino Mashaka.