Wakati mashabiki wa Simba SC wakitamba viongozi wao wanawasajilia mtu wa kazi, Aubrey Maphosa Modiba (28) kutoka Mamelodi Sundowns, huo siyo mpango wa Kocha Abdelhak Benchikha, ambaye amehamia upande wa Mohammed Hussein Tshabalala
Ishu ya Modiba anayecheza kama kiungo wa kushoto ama beki wa kushoto, imeshika kasi kwenye mitandao ya kijamii. kwamba viongozi wa Simba SC wamekwea pipa, kwenda kuzungumza na staa huyo anayetajwa ni miongoni mwa Top 10 kwenye Ligi Kuu Afrika Kusini kwa kuvuta mkwanja mrefu.
Hata hivyo, chanzo cha ndani ya Simba SC kinasema Benchikha amependekeza mabeki wawili wa kushoto akitaka wasajiliwe mmoja wapo wa kusaidiana na, Tshabalala.
Inadaiwa beki wa kwanza ni Ibrahim Imoro (24), raia wa Ghana anaichezea A-Hilal ya Sudan mbali na kucheza nafasi ya Tshabalala ana uwezo wa kucheza kiungo ya pembeni.
Beki mwingine ni Hernest Briyock Malonga (21), kutoka klabu ya Diables Noirs Brazzaville, huyo ni raia wa Congo.
Endapo mmoja wapo wa mabeki hao akifanikiwa kusainiwa Simba SC, haitakuwa kazi rahisi kumuweka Tshabalala benchi, ambaye ana uzoefu mkubwa kwenye mechi za Ligi Kuu na michuano ya CAF.
Tshabalala ana misimu 10 ndani ya Simba, tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Kagera Sugar, ameisaidia kunyakua mataji ya Ligi Kuu lakini pia akiipeleka Robo Fainali ya michuano ya CAF mara tano.