Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Julieth Mwakanyamale ambaye ni Mkaguzi Kata wa Kata ya Ngangokolwa, amewataka wananchi kutokuwa na mawazo hasi kuhusu Dawati la Jinsia na Watoto kwa kujenga dhana kuwa dawati hilo wanufaika ni Watoto na Wanawake na si Wanaume.
Mwakanyamale ameyasema hayo katika mahojiano maalum na kituo kimoja cha Radio kilichopo Wilayani Bariadi na kuongeza kuwa Dawati hilo ni la Wananchi wote na halibagui hivyo wasisite kufika kwa ajili ya huduma kwa dhana kuwa lipo maalum kwa ajili ya watu fulani.
“Ni fikra potofu kudhani dawati ni kwa ajili ya Wanawake na Watoto pekee, lipo kwa ajili ya watu wote na kama kuna Mwanaume anapitia changamoto za ukatili basi kama ataripoti ni lazima zitafanyiwa kazi,” alisema.
Amesema, mnufaika wa huduma za Dawati la Jinsia na Watoto ni mtu yoyote yule, hivyo kuwataka wanaume watoe taarifa za ukatili wa kijinsia ambazo wanafanyiwa na wenza wao, ili hatua stahiki zichukuliwe.
Itakumbukwa kuwa mapema mwaka huu (Januari 2023), baadhi ya wanaume na wanawake Katika Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, wamelalamikia ukatili wa kupigwa na wenza wao wa ndoa na kusababisha ndoa nyingi kuvunjia kwa kupeana talaka huku watoto wakiathirika na vitendo vya ukatili kwa kukosa malezi bora ya wazazi.