Kocha Mpya wa Dodoma Jiji, Francis Baraza amesema kusimama kwa Ligi Kuu Tanzania Bara, kutamsaidia kupata muda mzuri wa kukiimarisha kikosi chake ili kiwemo katika mbio za kusaka ubingwa msimu 2023/24.
Kocha huyo kutoka nchini Kenya amesema lengo lake ni kuifanya timu hiyo kutoa upinzani na kupata matokeo mazuri ili kutimiza malengo waliyojiwekea.
“Malengo ya timu ni kumaliza nafasi nne za juu na hilo linawezekana sababu tuna timu nzuri lakini kuna mapumziko ya muda mrefu nitatumia kipindi hiki kuhakikisha Dodoma Jiji inakuwa timu shindani,” amesema Baraza.
Pia amesema katika kipindi hiki amepanga timu iwe inafanya mazoezi mara mbili kwa siku na kucheza mechi nyingi za kirafiki ili kuifanya timu kuendelea kuwa katika ushindani.
Amesema amezungumza na wachezaji pamoja na uongozi kuwapa ratiba nzima na anashukuru kila mmoja amemuelewa na anaamini watatumia vizuri muda huo kwa lengo la kufanya timu hiyo kuwa bora zaidi.
Amesema anatambua ushindani uliopo, lakini watapambana ili kuhakikisha ndoto zao za kumaliza msimu huu ndani ya nne bora zinatimla.
Dodoma liji ipo nafasi ya saba kwenye msimamo ikikusanya pointi 18 katika michezo 14 waliyocheza hadi kufikia sasa.