Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ amegomea mkataba wa mwaka mmoja, huku akiutaka Uongozi wa Simba SC kumpa mkataba wa miaka miwili.
Saido ni kati ya wachezaji ambao mikataba yao imebakisha miezi sita ya kuendelea kubakia Simba SC, ambayo imepanga kufanya maboresho makubwa ya kikosi chao msimu buu, ambao wamepanga kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kiungo huyo alijiunga na Simba SC wakati wa Dirisha Dogo msimu uliopita, akitokea Geita Gold ambako alisaini mkataba wa miezi sita kabla ya kutua Msimbazi.
Zipo baadhi ya timu zinatajwa kuwania saini ya kiungo huyo, ambaye msimu uliopita alitwaa Ufungaji Bora akipachika mabao 17, sawa na aliyekuwa Mshambuliaji wa Young Africans aliye Misri kwa sasa sasa, Fiston Mayele. Kati ya hizo APR ya nchini Rwanda ndiyo imeonekana kuonyesha nia kubwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba SC, Saido amegomea mkataba wa mwaka mmoja aliowekewa mezani na badala yake, ameomba miaka miwili.
Mtoa taarifa huyo amesema kuwa kiungo huyo amesimamia misimamo yake, ya kugomea ofa hiyo ya mkataba mdogo huku akishinikiza kuongezewa mmoja ili ifikie miaka miwili.
“APR wameonesha nia ya kuhitaji saini ya Saido, ambaye amebakisha mkataba wa miezi sita ya kuichezea Simba SC, lakini ipo ofa ya mwaka mmoja ambayo amewekewa Simba SC.
“Ofa hiyo ameikataa, akiomba apewe mkataba wa miaka miwili, hivyo bado mazungumzo yanaendelea kati ya Simba SC na Saido juu ya mkataba huo mpya, licha ya kuwepo uwezekano mdogo wa kuongezewa.
“Simba SC wameonekana hawapo tayari kumuongezea mkataba huo, hivyo upo uwezekano mkubwa wa kuondoka klabuni hapo kwenda APR ambayo imempa ofa kubwa,” amesema mtoa taarifa huyo.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally, amezungumzia hilo la usajili na kusemna: “Hatima ya Saido ipo mikononi mwa kocha wetu Benchikha (Abdelhak) ambaye yeye ndiye anayesimamia usajili, hivyo ripoti yake ndiyo itakayoamua.”